Pages

Saturday

Serikali yapata gawio la Sh bilioni 1

KAMPUNI ya Kuhifadhi Mafuta nchini (TIPER) imekabidhi hundi ya Sh bilioni 1 kwa Serikali, ikiwa ni sehemu ya gawio la Serikali katika faida iliyotengenezwa hadi kufikia Desemba 31, mwaka jana. Kampuni hiyo inamilikiwa kwa ubia baina ya Serikali na Kampuni ya Uswisi ya Oryx (OOG), kila moja ikiwa na hisa 50, imekuwa ikilipa gawio kama hilo tangu mwaka 2009 baada ya uwekezaji wa Sh bilioni 8.3 ambao uliwezesha kufanya kazi kwa faida.


Kampuni hiyo ililipa gawio la Sh bilioni 1.3 mwaka 2009, bilioni moja katika mwaka 2010 na bilioni 2 katika mwaka 2011.

Akizunguzuma wakati wa hafla fupi ya kukabidhi hundi hiyo jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa wiki, Mkurugenzi Mtendaji wa TIPER, Daniel Belair, alisema mchango wa gawio toka katika kampuni hiyo utakuwa chachu ya maendeleo ya uchumi nchini.

“Tunayo furaha kukabidhi hundi hii yenye thamani ya shilingi bilioni 1 ikiwa ni wajibu wetu kisheria kama kampuni. Tunaamini mchango wetu utasaidia kuchochea mchakato wa maendeleo ya uchumi wa taifa kwa ujumla,” alisema Belair.

Alisema TIPER inatarajia kuongeza zaidi uwezo wake wa kuhifadhi mafuta ili kufikia zaidi ya mita za ujazo 290,000 ifikapo mwaka 2015, baada ya uwekezaji wa Dola za Marekani bilioni 12.

Belair alisema hadi sasa TIPER ina kituo kikubwa cha kuhifadhi mafuta nchini chenye uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo zaidi ya 141,000, ikilenga kufikia mita za ujazo 215,000 kwa siku za baadaye.

“Katika uwekezaji mpya, tenki mbili zenye uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo 36,600 zimeshaongezwa katika robo ya kwanza ya 2013. Kipaumbele chetu kikubwa ni kuhakikisha kuwa bidhaa za mafuta ya petroli zinapatikana katika soko muda wote,” alisema.

Alisema katika mwaka wa fedha wa 2011/2012, kampuni yake ilijikita katika miradi mbalimbali ya kusaidia jamii katika sekta za elimu na afya, ikiwa ni sehemu ya sera ya kampuni yake ya kusaidia jamii inayoizunguka kampuni.

Akipokea hundi hiyo kwa niaba ya Serikali, Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, aliitaka kampuni ya TIPER iendelee kufanya kazi kwa juhudi na kuihakikishia bodi ya kampuni hiyo kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada zake.

“Tuna furaha kwa kupata mchango huu wa gawio, kwani ni wakati muafaka. Msisite kuifuata wizara yangu kwa jambo lolote linalohitaji msaada wetu,” alisema

BONGO NEWS 4 NEWS#

No comments:

Post a Comment