Pages

Wednesday

Anayetuhumiwa kutaka kuua mumewe asota jela - Arusha/Arumeru.


JANETH Jackson (32), anayedaiwa kula njama za kutaka kumuua mumewe, Simon Jackson na mtoto wa mume huyo, ameendelea kusota mahabusu kwenye gereza la Kisongo ambapo wakili wake, Samson Rumende amepeleka maombi Mahakama Kuu akipinga mteja wake kunyimwa dhamana.
 
Wakili huyo aliwaeleza waandishi wa habari nje ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kuwa alipeleka maombi hayo chini ya hati ya dharura wiki mbili zilizopita baada ya kutoridhika na uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kumnyima dhamana mteja wake wakati kosa linalomkabili lina dhamana.
Alisema kuwa baada ya kufuatilia ameambiwa jalada la shauri hilo liko kwa jaji SC Moshi ambaye alithibitisha kuyapokea ambapo anayapitia kisha atapanga tarehe kwa ajili ya kuyasikiliza baada ya kuziarifu pande zote zinazohusika na shauri hilo.
Awali Janeth, mkazi wa Moshono, Arusha na Novatus Elias, walifikishwa mbele ya Hakimu 
Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha/Arumeru, Devotha Kamuzora, na kusomewa mashitaka mawili ya kula njama ya kutaka kumuua Jackson ambaye ni mfanyabiashara maarufu wa madini aina ya tanzanite.
Mwendesha mashtaka wa serikali, Edna Kasala, aliieleza mahakama hiyo katika shtaka la pili kuwa washtakiwa wote kwa pamoja walikula njama na kutaka kumuua Desderi Sabas, ambaye ni mtoto wa mke mwingine wa Jackson anayeishi Bukoba, mkoani Kagera.
Washtakiwa wote hawakutakiwa kujibu lolote kwa sababu mahakama hiyo kisheria haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.
Mwendesha mashtaka huyo aliiomba mahakama kuwanyima dhamana washtakiwa, kwa sababu upelelezi haujakamilika kwani kuna watuhumiwa wengine wawili wanatafutwa hivyo kutokana na uzito wa tuhuma hizo, maombi hayo ya kuwanyima dhamana yaliambatanishwa na hati ya kiapo ya mkuu wa upelelezi makosa ya jinai Mkoa wa Arusha.
Kwa upande wake, aliyekuwa wakili wa utetezi, Fidelis Peter, alipinga maombi hayo na kutaka mahakama itoe dhamana kwa washtakiwa kwa sababu ni haki yao ya kikatiba na kwamba hilo ni kosa lao la kwanza na kuitaka mahakama kupuuzia hoja za Jamhuri kuwa washtakiwa watavuruga upelelezi wakiachiwa hazina msingi.
Aliendelea kusema kuwa mshtakiwa wa kwanza, Janeth ana mtoto wa miezi sita na tangu akamatwe hajamwona wala kumnyonyesha, hivyo anastahili kupewa dhamana.
Hata hivyo, baada ya kusikiliza maombi ya pande zote mbili, hakimu Kamuzora alikubaliana na maombi ya upande wa mashtaka na kuamuru watuhumiwa wapelekwe mahabusu hadi Agosti 5, mwaka huu.

BONGO NEWS 4 NEWS#

 
 

No comments:

Post a Comment