
Timu hiyo tajiri yenye kila kitu kinachostahili
kuitwa timu ya kisasa ya kulipwa, imejipanga kivingine tayari kwa msimu
mpya. Msisitizo wa kocha ukiwa ni kuchukua kombe na kushiriki Ligi ya
Mabingwa Afrika kwa vile Shirikisho sasa imetosha.
Kocha huyo Mwingereza, Sterwart Hall hakufanya
mabadiliko kwenye kikosi chake lengo likiwa ni kuendeleza makali
waliyoanza msimu uliokwisha. “Nataka kufanya vizuri zaidi ya msimu
uliopita na kuvunja rekodi ya mwaka uliopita, ndiyo malengo yetu,”
anasema Stewart ambaye timu yake ndiyo klabu pekee ya Tanzania
iliyokwenda Afrika Kusini kwa mechi za kirafiki na ilidumu huko kwa siku
kumi.
Katika mechi za huko, safu ya ushambuliaji ndiyo
iliyomwangusha kwa kushindwa kufunga mabao mengi jambo ambalo
linaonekana kuwa ni tatizo kwenye kikosi hicho. “Mabao ni tatizo, lakini
tutacheza na hesabu tu pamoja na mazoezi na kufanikisha malengo yetu na
kila mchezaji atafunga,” anafafanua.
Azam, ambayo Jumamosi iliyopita ilikubali kipigo
cha bao 1-0 kutoka kwa Yanga katika mechi ya Ngao ya Jamii, itaanza ligi
bila wachezaji wake wa kimataifa, raia wa Kenya, Humphrey Mieno
anayeumwa nyama za paja na Brian Umony raia wa Uganda anayeuguza maumivu
ya enka.
Kikosi cha Azam
Azam ipo chini ya Mkurugenzi Aboubakary Bakhresa na makazi yao
ni Chamazi, Mbande, jijini Dar es Salaam, ina miaka sita tangu
ilipoanzishwa lakini imekuwa tishio kwa wakongwe Simba na Yanga.
Kwa misimu miwili mfululizo mwaka juzi na mwaka
jana, iliwapangua wakongwe hao, ikawaweka pembeni na kung’ang’ania
nafasi ya pili kwenye ligi na kuliwakilisha Taifa mara mbili Kombe la
Shirikisho.
Pia, licha ya ugeni wao huo ndiyo klabu pekee
Tanzania inayomiliki uwanja wao binafsi wa kisasa wenye ‘pichi mbili’,
moja nyasi bandia na mwingine una nyasi asilia pamoja na hosteli. Mtibwa
ndiyo klabu nyingine yenye uwanja binafsi wenye nyasi asilia. Hali
hiyo inaifaidisha Azam ambayo itacheza mechi nyingi zaidi kwenye uwanja
wao wa nyumbani ambao pembeni kidogo zipo hosteli zao zinazotumika kwa
kambi.
Stewart anasaidiwa na Kalimangonga Ongala pamoja
na Mkenya, Ibrahim Shikanda kwenye benchi la ufundi. Kocha Stewart
ambaye kwa hulka yake ni mcheshi, amebainisha kuwa mfumo anaopenda
kuutumia ni 4-3-3 ingawa mara nyingine ni 4-2-3-1 na 4-1-2-3.
Nahodha wa timu ni John Bocco ‘Adebayor’ na Himid
Mao ndiyemsaidizi wake. Straika, Gaudence Mwaikimba, ndiye mchezaji
mrefu kuliko wote na Salum Aboubakary ‘Sure Boy’ ni mchezaji mfupi
kuliko wote katika kikosi hicho.
Azam itatumia jezi za nyumbani rangi nyeupe na ugenini ni bluu na njano.
Azam haijafanya usajili wowote, lakini imewapandisha wachezaji
wanne kutoka timu B ya vijana chini ya miaka 20 ambao ni kipa Aishi
Manula, Mudhahir Yahya, Hamad Kadili na Dismas.
Wachezaji wa kimataifa ni pacha kutoka Ivory
Coast, Kipre Tchetche na Kipre Bolou, Wakenya Mieno na Jockins Atudo
pamoja na Brian Umony raia wa Uganda.
Wazawa ni Mwaikimba, Himid, Ibrahim Mwaipopo,
Jabir Aziz, Bocco, Khamis Mcha, Luckson Kakolaki, Mwadini Ally, Said
Morad, Marika Ndeule, David Mwantika, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Sure
Boy, Samih Haji, Waziri Salum na Seif Karihe.
No comments:
Post a Comment