.
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), manispaa ya Ilemela, mkoani Mwanza, kimeitisha maandamano makubwa ya amani leo kwa ajili ya kushinikiza kung’olewa kwa meya wa manispaa hiyo, Henry Matata, anayedaiwa kuchaguliwa kinyume cha sheria
Akitangaza maandamano hayo mbele ya waandishi wa habari jijini hapa
jana, Ofisa Operesheni wa CHADEMA Kanda ya Ziwa Magharibi, Tungaraza
Njugu, alisema yataungwa mkono na maelfu ya wananchi wa Nyamagana.
Alisema maandamano hayo yataanzia Buzuruga saa 4:00 asubuhi kisha
kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo, katika uwanja wa
Furahisha, na kwamba unahitajika kufanyika upya uchaguzi wa meya na
naibu wake.
Tungaraza aliyeongozana na ofisa wa chama kanda hiyo, Meshack Mikael,
pamoja na katibu wa mbunge wa Ilemela, Laban Agrey, alisema maandamano
hayo yanahusisha pia kupinga kufukuzwa kinyemela madiwani watatu wa
chama hicho.
Madiwani waliofukuzwa na meya wa manispaa hiyo kinyume cha sheria ni
Abubakar Kapera (Nyamanoro), Malietha Chenyenge (Ilemela) na Dany
Kahungu wa kata ya Kirumba.
“CHADEMA tumeitisha maandamano makubwa hapo kwa lengo la kumkataa meya wa Ilemela na kushinikiza uchaguzi ufanyike upya.
“Matata amechaguliwa bila kukidhi akidi ya madiwani wa manispaa hiyo
ambayo ni theluthi mbili ya madiwani wote 14, hivyo siyo meya.
“Lakini maandamano haya yatalenga pia kupinga Matata kuwafukuza
madiwani wetu kinyemela. Sheria zinasema diwani atakosa sifa baada ya
kutohudhuria mfululizo vikao vitatu vya Baraza la Madiwani, lakini
Matata aliyechaguliwa kinyume cha sheria aliwafukuza ndani ya wiki moja
baada ya kuchaguliwa,” alisema.
Alisema CHADEMA pamoja na wananchi wa Ilemela wanahitaji kufanyika
upya kwa uchaguzi wa meya na naibu wake na kwamba kama kweli madiwani
hao wamefukuzwa kihalali wapewe barua za kufukuzwa kwao na tume ya
uchaguzi itangaze kata hizo kuwa wazi.
“Kuna taarifa zinaeleza kwamba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,
alishaandika barua ya kutengua uamuzi wa kufukuzwa madiwani hao na barua
hiyo ‘imekaliwa’ na mkuu wa mkoa,”alisema.
Naye katibu wa Highness Kiwia, Laban Aggrey, kwa niaba ya mbunge huyo
alisema kuwa maandamano hayo yataanzia Buzuruga kisha kupita barabara ya
Nyerere, Mlango mmoja, Uhuru, Nkrumah, Balewa na kuishia uwanja wa
Furahisha.
“Polisi wameshabariki kufanyika maandamano yetu, hivyo ofisi ya mbunge
wa Ilemela inawasihi sana wananchi wajitokeze kwa wingi kuja kudai haki
yao iliyoporwa kinyume cha sheria,” alisema.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,
Ernest Mangu, alisema maandamano hayo ya CHADEMA yameruhusiwa na jeshi
lake.
“Haya maandamano tumeyaruhusu kabisa yafanyike, maana kama watu
wanasema wanadai haki yao kwa nini tuwazuie? Tumewapangia maeneo ya
kupita maandamano haya hadi huko Furahisha,” alisema Mangu.
Uchaguzi wa meya wa Ilemela uliofanyika Desemba mwaka jana, ulikiuka
kanuni na sheria za halmashauri, ambapo akidi ya wajumbe iliyokuwa
ikihitajika kwa ajili ya meya kupigiwa kura ni madiwani tisa, lakini ni
madiwani sita tu ndiyo waliopiga kura.
Katika uchaguzi huo uliohudhuriwa na mkuu wa wilaya hiyo, Amina
Masenza (DC), pamoja na mwanasheria wa jiji la Mwanza, Savela Manzi,
aliyesimamia uchaguzi huo kwa upande wa mambo ya sheria, Matata
alitangazwa kuwa meya baada ya kuchaguliwa na madiwani wasiokidhi
theluthi mbili.
Madiwani waliopiga kura kumchagua Matata na naibu wake (Dede Swila wa
CCM), walikuwa wanne wa CCM, mmoja wa CUF ambaye ni mbunge wa viti
maalumu, Mkiwa Kimwanga, na Matata mwenyewe aliyefukuzwa uanachama wa
CHADEMA.
Matata alichaguliwa wakati suala lake la kufukuzwa uanachama ndani ya CHADEMA likiwa bado linangojea uamuzi wa mahakama.
Credit:Tanzania Daima.
No comments:
Post a Comment