Pages

Tuesday

WILAYA ya Arumeru mkoani Arusha kujenga uwanja wa kisasa wa soka.

WILAYA ya Arumeru mkoani Arusha iko mbioni kujenga uwanja mkubwa wa kisasa wa soka ikiwa ni mpango mkakati wa kuendeleza michezo wilayani hapa baada ya kufanikiwa kuwa na timu nyingi za vijana.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya hiyo (DC), Nyerembe Munasa, wakati akizungumza katika hafla ya utoaji zawadi kwa mabingwa wa ligi maalumu ya vijana Arumeru, iliyoanzishwa na mdau wa michezo kutoka nchini Ufaransa, Damian Sellier, katika mji mdogo wa Usa River, eneo la Liganga.
DC Nyerembe alisema, hiyo ni mikakati yake katika kukuza michezo kwa kushirikiana na Halmashauri ya Meru, ambako tayari eneo la ujenzi limepatikana na kinachofuata ni mipango ya ukusanyaji fedha kwa ajili ya ujenzi huo kuanza.
Alifafanua kuwa katika mpango huo, kabla ya ujenzi kukamilika, hivi sasa wataanzisha mashindano ya vijana wadogo kutafuta vijana 20 bora, ambao watakuwa waanzilishi wa timu maalumu ya wilaya, ambayo mwakani itapelekwa nchini Brazil kwa ajili ya mafunzo maalumu.
“Tayari nimeishapata baadhi ya wadhamini kusaidia mpango wa kukuza soka kwa vijana na tumekubaliana kuanzia na vijana 20, ambao watapelekwa nchini Brazil kwa ajili ya mafunzo maalumu, ili wakirudi wawe ndio mfano kwa soka la nchi hii,” alisema Munasa.
Aidha, kupitia Halmashauri ya Meru, waliahidi mara baada ya kumalizika kwa mashindano hayo juzi, wataanza kuukarabati uwanja wa Ngarasero, kwa kuukwangua na kuweka udongo mpya kisha kupanda majani ili uwe na hadhi stahiki kutumika katika mechi mbalimbali.
Naye Mratibu wa kituo cha Usa River Youth, ambao ndio walikuwa wasimamizi wa ligi hiyo, Daudi Mkumba, licha ya kumshukuru DC Nyerembe na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru kwa ushirikiano wao, aliwaomba kuhakikisha wanatoa ushirikiano zaidi kwa taasisi zinazoanzisha mashindano ya vijana ili kukuza na kuibua vipaji.
Katika mashindano hayo, timu ya Charky U-20 na ile ya U-15 waliibuka mabingwa na kuambulia kombe na mipira, kabla ya DC Nyerembe kutoa sh 200,000.
BONGO NEWS 4 NEWS#


No comments:

Post a Comment