Pages

Saturday

Kortini kwa kughushi saini ya Pinda...ni MFANYABIASHARA Amadi Ally Popi (35).


Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
 Habari na Happiness Katabazi
MFANYABIASHARA Amadi Ally Popi (35), jana alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, akikakabiliwa na makosa mawili likiwemo la kughushi barua inayoonyesha imeandikwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Mbele ya Hakimu Mkazi Waliarwande Lema, Inspekta wa Polisi Hamis Said alidai tarehe na siku isiyofahamika ndani ya jiji la Dar es Salaam, kwa nia ya kudanganya Popi alighushi barua yenye kumbukumbu Na,DA21/3078/01A/142 ya Desemba 3, 2012 akijaribu kuonyesha kuwa barua hiyo ni halali na ilikuwa imeandikwa na kusainiwa na Waziri Mkuu, Pinda.
Alidai shtaka lingine ni kuwa tarehe na siku isiyofahamika ndani ya jiji la Dar es Salaam, bila ya kuwa na mamlaka yoyote alitengeneza barua hiyo na kuisani na kisha alimpatia Islamu Mohammed Mtila akijaribu kuonyesha barua hiyo imetoka katika Ofisi ya Waziri Mkuu na imesainiwa na Pinda.
Mshtakiwa huyo alikana tuhuma hizo na kupelekwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili wanaofanya kazi serikalini au kwenye taasisi zinazofahamika watakaosaini bondi ya sh milioni 10.
Pia mmoja wa wadhamini hao kuwasilisha mahakamani hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo. Kesi itatajwa Septemba 5 mwaka huu kwa kuwa upepelezi wake haujakamilika.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la  Jumamosi Agosti 24 mwaka 2013.
BONGO NEWS 4 NEWS#

No comments:

Post a Comment